Wakati mchakato wa kumpata mzabuni atakayetengeneza kadi maalumu za abiria wa mabasi ya mwendokasi Dar es Salaam (Udart) ukiendelea, Mtendaji Mkuu wa mradi wa mabasi hayo (Dart), Ronald Lwakatare amesema kadi 60,000 ndizo zinazotumika.

Katika siku za karibuni kadi za mabadi hayo zimeadimika kiasi cha wananchi kuhoji juu ya suala hilo, lakini uongozi wa Dart ukadai kuwa linashughulikiwa kwa kusaka mzabuni akayekabidhiwa jukumu hilo.

Hata hivyo, jana, Lwakatare alisema kati ya kadi 200,000 zilizonunuliwa na Serikali kwa ajili ya kutumika kwenye mfumo wa mabasi hayo ni kati ya kadi 50,000 hadi 60,000 zinazoonekana kutumiwa na wananchi.

Alisema kadi ambazo zinatumika kwa sasa ni sawa na asilimia 25, huku asilimia 75 zikiwa mifukoni mwa wateja ambao miongoni mwao wamo walichukua kadi mara mbili.

Lwakatare alisema kutotumika kwa kadi hizo kumechangia kuwepo kwa misururu ya abiria kwenye vituo vya mabasi yaliyopo kwenye mfumo huo. “Kusudi ni kwamba kadi moja kwa mtu mmoja, lakini inaonekana mtu mmoja anamiliki kadi zaidi ya moja jambo ambalo si sahihi,” alieleza.

Alifafanua kwamba wakati wa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo Serikali ilinunua kadi 200,000 kutokana na makadirio iliyoyafanya kabla ya kuanza kutoa huduma na zilipaswa kutumiwa na wananchi wanapohitaji kusafiri, lakini imebainika kwamba nyingi ya kadi hizo hazitumiki.

Kufuatia hali hiyo, mtendaji huyo mkuu aliwataka wananchi wanaomiliki kadi hizo wazitumie ili kurahisisha usafiri kwa kuwa ndizo zilizokusudiwa kutumika.

Aliongeza kuwa, kulingana na takwimu zilizopo wananchi kati ya 200,000 hadi 250,000 ndio wanaotumia huduma ya usafiri huo kila siku na kwamba, endapo kadi hizo zingekuwa zinatumika kusingekuwa na msururu wa abiria kukata tiketi.

Kwa upande wao, baadhi ya abiria wanaotumia mabasi hayo walisema kadi nyingi zinaweza kuwa zimepotea.

“Nimeshapoteza kadi mbili na hii niliyonayo ni ya tatu. Lazima Serikali iweke mfumo wa kuandaa nyingine kama ilivyo kwa kadi za benki, ikipotea unapewa nyingine kwa namba ileile,” alisema mkazi wa Kimara, Lusiana Ng’onze.

Joachim Jones anayeishi Ubungo alisema kama ingeanzishwa sheria ya kutumia na kuzitunza kadi hizo watu wengi wangezitunza.

0 comments:

Post a Comment

 
Top
CelebritySwaggz.Com