Hii Hapa ni Gharama ya Matibabu iliyotumika Kuokoa Uhai wa Tundu Lissu
Wakati habari za shambulio la risasi dhidi ya Tundu Lissu zikihamia kwa viongozi wa kidini, Chadema imeeleza gharama zilizotumika hadi sasa kuokoa maisha yake na kuweka bayana kuwa imemuhamishia dereva wake nje ya mipaka kumuepusha na waliofanya shambulio hilo.

Lissu, mwanasiasa ambaye hana woga wa kuzungumza analoamini, alishambuliwa kwa risasi zipatazo 32 wakati akiwa kwenye gari lake lililoegeshwa nje ya majengo ya nyumba anayoishi akiwa Dodoma wakati wa shughuli za Bunge.

Risasi tano zilimpata mwilini, lakini akaepuka kifo na kwa sasa amelazwa Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi, ambako hali yake imeelezwa kuwa nzuri.

Taarifa ilkiyotolewa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana jioni pia imeeleza sababu za kumhamishia Lissu Hospitali ya Aga Khan ya jijini Nairobi, Kenya kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na kushukuru wote waliohusika kuokoa maisha yake.

“Maisha ya Mhe Lissu yalikuwa hatarini sana na palihitajika matibabu maalumu na ya haraka sana kutoka kwa madaktari bingwa,” inasema taarifa hiyo.

Imeongeza kuwa matibabu yake pia yalihitaji vifaa tiba visivyo na shaka yeyote ili kuokoa maisha yake baada ya “kazi na kubwa na ya kupongezwa ya awali iliyofanywa na madaktari wetu kadhaa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma”.

Imeongeza kuwa jana, Lissu alikuwa akifanyiwa upasuaji mwingine.

“Hofu kuu ya usalama wa Mhe Lissu na dereva wake ilitanda kote nchini Tanzania baada ya shambulio dhidi ya uhai wao kushindwa kufanikiwa,” anasema Mbowe katika taarifa hiyo.

“Busara ya kiusalama ilitulazimisha kuwatoa wahanga nje ya mipaka ya nchi hadi hapo usalama wao utakapohakikishwa.

Mbowe anasema shambulio hilo lilimuumiza sana Lissu na ameokoka kimiujiza.

“Kutokana na ukweli huu, matibabu yake vilevile ni maalum na yanayohitaki wataalam wengi, vifaa tiba maalum na gharama kubwa,” anasema.

“Hadi sasa, zaidi ya Shi100 millioni zimeshatumika kuokoa maisha ya ndugu yetu Lissu.

“Thamani ya Mhe. Lissu, ni kubwa kuliko kiwango chochote cha fedha. Kila njia iliyo halali itatumika kupata fedha za kutosha kumtibu Mhe. Lissu na hatimaye kumrudisha kwenye uwanja wa kudai haki, demokrasia na ustawi kwa wote nchini Tanzania.”

Taarifa hiyo inasema “dereva wa Mhe. Lissu, Simon Mohamed Bakari naye tunaye hapa Nairobi akiendelea kupata huduma za kisaikolojia”.

“Alishuhudia shambulio lile na aliokoka kimiujiza. Anasumbuliwa na msongo mkubwa wa mawazo. Naye hatukuona busara kuendelea kumuacha nchini hadi hapo hali yake ya kiafya na kiusalama itakapohakikishwa,” anasema Mbowe.

“Ni dhahiri kwa aina ya shambulio lilivyokuwa, wauaji walikusudia kuwaua wote; Mhe. Lissu na hata dereva wake.”

Chadema imerejea mazungumzo baina ya Serikali na chama hicho kuhusu hospitali gani apelekwe kutoka Dodoma.

“Upande wangu na Wabunge wetu wa Ukawa ulisisitiza Mhe. Lissu apelekwe moja kwa moja Nairobi na kama Bunge na Serikali hawatakuwa tayari kubeba gharama za kuokoa maisha ya Mhe. Lissu, basi sisi na Watanzania wenye mapenzi mema watachangia gharama hizo za kuokoa maisha kitibabu na kiusalama,” amesema Mbowe.

Mbowe amesema Lissu alitibiwa na madaktari wapatao kumi wa fani tofauti baada ya kufika Nairobi na walifanya kazi hiyo usiku kucha na anaendelea kutibiwa muda wote akiwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu, lakini juzi aliweza kuzungumza.

“Kwa mara ya kwanza, Mhe. Lissu aliongea jana jioni na mkewe Alucia na baadaye na mimi, akisema ‘mwenyeki, I survived to tell the tale (niliokoka ili nisimulie mkasa). tafadhari, endeleeni kupambana”.

Amesema watu kutoka sehemu mbalimbali wamekuwa wakitaka kumtemebelea, lakini hawaruhusiwi na ulinzi umeimarishwa katika eneo analotibiwa.

“Hairuhusiwi wageni kumuona hadi hapo madaktari wakiridhika kuwa hali yake ya kimatibabu inaruhusu,” alisema.

Chadema imeeleza katika taarifa hiyo kuwa Tanzania si Salama, ikirejea mauaji ya mwenyekiti wa chama hicho mkoani Geita, Alphonce Mawazo aliyeuawa mwaka 2015, kamatakamata za wanaharakati na kuteswa kwa kilichoitwa makosa ya kimtandao.

Pia imetaja kutoweka kwa mshauri wa Mbowe, Ben Saanane na kutekwa kwa wasanii na kuteswa; kutaifishwa kwa mali, mashamba na biashara za viongozi wa upinzani.

Viongozi wa dini

Jana, viongozi wa kidini waliungana na watu wengine kuendelea kulaani shambulio hilo na kumuombea Lissu arudi katika hali yake.

“Naomba tusimame kidogo nizungumze jambo, nimesema leo nitakuwa na ibada maalumu ya kumuombea Lissu,” alisema Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima wakati wa mahubiri yake jana.

“Somo langu la leo linasema damu isiyo na hatia.”

Gwajima, ambaye alisema ataenda Nairobi leo kumjulia hali Lissu, alisema kama kiongozi wa dini hatasita kukemea tukio hilo.

Alisema neno la Mungu linasema atakayemwaga damu ya mwanadamu mwenzake, damu yake naye itamwagika vivyo hivyo na kwamba “damu inayomwagika chini ya ardhi ina sauti, inamlilia Mungu”.

Kabla ya Gwajima kuzungumza, wanakwaya wa kanisa hilo waliimba wimbo maalumu wa kumuombea Lissu wakihamasisha Taifa lote kufanya hivyo.

Baadhi ya maneno yaliyo katika mashairi ya wimbo huo yanasema “amani ya Tanzania inapotea, wasione tuko kimya; kwa nini haya yanatokea na watu wasiojulikana; Watanzania wote tumuombee Lissu”.

Mdogo wa Lissu azungumza

Katika ibada hiyo alikuwepo mdogo wa mbunge huyo anayeitwa Vincent Lissu na alipopewa fursa ya kuzungumza, alisema kabla ya kaka yake kushambuliwa kwa risasi aliwaeleza kwamba kuna mtu anafuatilia gari lake.

Hata hivyo, alitaka jamii na Jeshi la Polisi kutomtuhumu dereva wa Lissu kuhusika katika shambulio hilo.

“Nimesoma gazeti la leo la Mwananchi, ukurasa wa mbele unasema dereva wa Lissu asakwa na polisi. Nafikiri ni kitu cha kawaida tukio kama hilo linapotokea, uchunguzi lazima ufanyike,” alisema Vincent.

“Na kijana huyu alikuwepo. (Kwa hiyo) Katika mazingira ya kawaida, ni lazima aweze kuzungumza na polisi hicho ni kitu kizuri.

“Lakini sasa kwenye mitandao ya kijamii imeonekana kama huyu kijana ndiye anahusika. Mambo ya kisiasa yasifanye aonekane anahusika wakati alisaidia kumuokoa ndugu yangu. Simaanishi kama Mwananchi waliandika hivyo.”

Vincent alisema suala la kusaidia polisi kwa kutoa maelezo kwa kuwa yeye ndiye aliyeshuhudia ni jambo zuri, lakini wasimwingize kwenye suala la kuhusika katika tukio hilo.

“Hawa watu walitaka kumuua Lissu na suala hilo halikuweza kufanyika na huenda dereva aliwaona. Kwa hiyo si vizuri akawa wazi lazima ajifiche maana hao watu wanaweza kuja kumdhuru pia,” alisema.

Vincent alisema baada ya kaka yake kushambuliwa Alhamisi iliyopita, alienda Dodoma na alimuona akiwa amelala kitandani hospitalini mwili ukiwa na damu.

Aliwashukuru madaktari waliofanya kila waliloweza kuokoa maisha ya kaka yake aliyesema ni mpenda haki tangu akiwa mdogo.

Pia, aliwaomba wananchi wazidi kumuombea. Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea.

Vincent alisema alihudhuria ibada hiyo baada ya kuelezwa na mmoja wa waumini kuwa itakuwa ya kumuombea kaka yake.

Askofu Shoo atoa ya moyoni

Kiongozi mwingine wa kiroho aliyezungumzia suala hilo ni mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo, ambaye aliwataka watu waovu watambue kumuondoa Lissu mmoja,kutazalisha wengine maelfu.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu kutoka Bonn, Ujerumani jana, Askofu Shoo alitoa wito kwa Serikali kuhakikisha wote waliohusika wanakamatwa.

Hata hivyo, hadi jana jioni hakukuwepo na mtu aliyekamatwa, lakini juzi polisi mkoani Dodoma ilisema imekamata magari manane aina ya Nissan kwa ajili ya uchunguzi kutokana na wahalifu kudaiwa kutumia aina hiyo gari katika shambulio dhidi ya Lissu.

“Nimeshtushwa na kusikitishwa na taarifa za kupigwa risasi Mheshimiwa Tundu Lissu,” alisema Askofu Shoo.

“Watanzania tunapaswa kukataa na kulaani kwa nguvu zote vitendo kama hivi. Ninaamini kuwa nguvu zilezile za uovu zilizokuwapo tangu awamu zilizotangulia ndizo zinazoendeleza unyama kama huu. Ninamwomba Mungu ampe uponyaji wa haraka.

“Tundu Lissu amekuwa mstari wa mbele kufunua ufisadi unaoendeshwa na wababe wachache. Hawa sasa wanaona wameanza kutikiswa na kwa kuwa kwao wingi wa mali na pesa ndio mungu wao. Hatushangai wakitumia kila njia kuzuia ufisadi wao usianikwe hadharani. Watajaribu kila njia kuzuia ukweli, lakini wanasahau kuwa ukweli hauzuiliki milele, kuna siku utajitokeza tu.

“Kumuondoa Lissu mmoja, kutazalisha Lissu maelfu. Wito wangu kwa Serikali ya Dk (John) Magufuli ni huu, kwamba watu wote waliohusika wasakwe na wafikishwe mbele ya sheria.”

Dk Shoo, ambaye pia ni askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, alisema Serikali yoyote makini inajua namna ya kuulinda upinzani kwa kuwa ukitumika vizuri unakuwa kioo cha Serikali cha kujitazama.

Naye mwinjilisti kiongozi wa Mtaa wa Saranga ulio chini ya Usharika wa Temboni KKKT, , David Kawesa ameongoza maombi kumuombea Lissu.

“Mwenyezi Mungu, watu wasiojulikana ndio wamemjeruhi Lissu, imarisha afya yake tena,” alisema katika maombi yake.

“Wewe unayewajua hao wasiojulikana, wafunue. Tukio hili limetushtua tunaomba amani, uzidi kuitetea amani ya nchi yetu.”

Kiongozi mwingine wa kidini, Askofu wa zamani wa Kanisa la Pentekoste (FPCT), Paulo Samwel aliwasihi wananchi mkoani Singida na na Watanzania kuendelea kuwa na amani na utulivu kipindi hiki ambacho Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka waliomshambulia.

Askofu Samwel aliliambia gazeti hili kuwa polisi wana uwezo wa kuwasaka na kuwakamata wahusika ambao wanataka kuchafua nchi.

0 comments:

Post a Comment

 
Top
CelebritySwaggz.Com