Songombingo la ndoa ya jamaa aliyetobolewa macho na Scorpion, Said Mrisho na mkewe Stara Sudi ‘Mama D’ juzikati lilichukua sura mpya baada ya Said kumgeuzia kibao mkewe na kusema watoto mapacha waliozaliwa na mwanamke huyo anahisi siyo damu yake.

Awali akizungumza na kituo kimoja cha redio jijini Dar mwishoni mwa wiki iliyopita, Mama D alisema kuwa mumewe huyo aliwahi kukana mimba ya watoto hao lakini Said aliyekuwepo redioni hapo alikanusha na kusema kuwa, jamii ijue kuwa watoto ni wake hivyo akampa mkewe matumaini mapya.

Hata hivyo, Jumanne iliyopita Ijumaa liliibuka nyumbani kwa Said, Vingunguti jijini Dar anakoishi na yule mkewe Mwarabu na katika maelezo yake akasema, kauli yake kutoka moyoni ni kwamba anahisi wale watoto mapacha siyo wake.

“Jamani iko hivi, kabla sijapata ulemavu nilikuwa na miezi kama mitatu sijakutana na mke wangu, baada ya kupata matatizo nikawa na miezi mingine mitatu bila kukutana kimwili, baada ya kuishi kwa siku nyingi bila kukutana, siku tulipokutana tu wiki chache baadaye akaniambia ana mimba ya miezi minne!

“Ndiyo maana nasema nina wasiwasi na hawa watoto mapacha si wanangu. Haya yote sikutaka kuyasema tangu mwanzo kwa kuwa sikutaka mvutano na mwanamke huyo, wala sikuona kama ni vema kusema maovu yake mengi,” alisema Said.

Baada ya maelezo hayo, paparazi wetu alimvutia waya Mama D ambapo baada ya kumwagiwa maelezo ya Said alitokwa na povu ‘si la nchi hii’ huku akimuomba Mungu ampe mabalaa mzazi mwenzake huyo.

“Mungu amlaani maisha yake yote na niseme tu, natamani apate balaa kubwa kuliko hilo alilonalo, naona ulemavu umemfanya akili yake ishindwe kufikiri sawasawa.

“Ambacho naweza kusema ni kwamba, kama ana wasiwasi na hawa watoto anaweza kwenda kupima DNA akikuta watoto si wake, ruksa aniache nao, nitawalea peke yangu na kama vipimo vitaonyesha watoto ni wake naapa kwa jina la Mungu naenda kumtelekezea vichanga hivi mlangoni kwake awalee mwenyewe,” alisema mama D.

0 comments:

Post a Comment

 
Top
CelebritySwaggz.Com