RAPA chipukizi ambaye haishiwi vituko Harmorapa, amefunguka na kusema Alikiba ni msanii ambaye amekosa mfano hapa Tanzania kutokana kazi zake na namna ambavyo amekuwa akifanya mambo yake nje ya muziki.

Harmorapa amesema hayo siku chache baada ya Alikiba kudondoka wino na kampuni ya usimamizi wa kazi za wasanii RockStar4000 na kuwa Mkurugenzi wa muziki na vipaji  wa kampuni hiyo, pia kuwa sehemu ya wamiliki wa kampuni ya Rockstar4000 Music Entertainment Co & Rockstar Television.


“Katika vitu ambavyo tunatakiwa kujivunia ni kuwa na wasanii ambao wanatangaza taifa letu mbele na kujivunia juhudi zao. Naimani heshima, busara na juhudi ndiyo nyenzo pekee zilizowafanya wazungu kumwaga wino na kumkaribisha Alikiba meza moja na kumkabidhi kampuni kubwa ya Rockstar4000 kuwa mmiliki mmoja wapo na Director” alisema Harmorapa

Mbali na hapo Harmorapa aliwataka wasanii wengine kujifunza na kujivunia uwepo wa Alikiba kwani amekuwa akiutendea haki muziki wa bongofleva na kuipeperusha vizuri bendera ya Tanzania nje ya nchi.“Wasanii wa Tanzania inabidi tujifunze na kujisifu kwa kuwa na King Alikiba maana anautendea haki mziki wetu wa bongo fleva, hongera zangu zizidi kutiririka kwa King wewe uliokosa mfano hapa bongo” alisisitiza Harmorapa

Harmorapa ni kati ya wasanii ambao wamekuwa na mapenzi sana na Alikiba kwani mara kadhaa amekuwa mstari wa mbele kuonyesha mapenzi yake hayo kwa msanii huyo na kuonyesha jinsi gani anamkubali, kiasi cha kuhangaika sana japo aweze kufanya naye collabo, Harmorapa alishawahi kusema uongozi wake unahangaika kuona kama wanaweza kupata fursa ya kufanya kazi na Alikiba.

0 comments:

Post a Comment

 
Top
CelebritySwaggz.Com