SIMBA imeanza mazungumzo na straika wa Yanga, Donald Ngoma ambaye ameomba dola 80,000 sawa na Sh milioni 180 ili asaini mkataba wa kuichezea timu yao msimu ujao.

Kama Simba itafanikiwa katika dili hili la Ngoma raia wa Zimbabwe, itakuwa inamsajili mchezaji wa pili kutoka Yanga msimu huu kwani tayari inaye kiungo Haruna Niyonzima. Simba imenasa saini ya Niyonzima kwa dau la dola 60,000 (Sh milioni 132) na mshahara wa dola 3,000 sawa na Sh milioni 6.6.

Bosi mmoja wa Kamati ya Usajili ya Simba, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, tayari wamemfuata Ngoma na amewaambia wazi kuwa wampe dola 80,000 ili asaini mkataba wao wa miaka miwili.

“Tunafanya usajili kwa ajili ya Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi Kuu Bara msimu ujao, tunataka tufike mbali kwenye mechi za Caf (Shirikisho la Soka Afrika) pia tunataka ubingwa wa ligi yetu.

“Sasa ili tuwe na timu bora ni lazima tusajili vizuri, sasa tumemalizana na Niyonzima, tunaelekeza nguvu zetu kwa Ngoma tunayemuhitaji kwa ajili ya kuongeza nguvu.

“Ngoma anataka dola 80,000 ili asaini mkataba wetu, lakini sisi tutamuomba apunguze ili tukiafikiana tumpe hiyo fedha awe mchezaji wetu,” alisema bosi huyo kijana.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe hivi karibuni alililiambia gazeti hili kwamba, Niyonzima na Ngoma ni kati ya wachezaji anaowakubali na wana uwezo wa kuichezea timu yake.

Siku chache baada ya kauli hiyo ya Hans Poppe, kweli Simba ikamalizana na Niyonzima na sasa imeelekeza nguvu kwa Ngoma, straika anayesifika kwa ufungaji huku akimudu kutumia nguvu na akili uwanjani.

Imeelezwa kuwa, Simba imepata jeuri ya fedha iliyowawezesha kumbakisha kikosini nahodha Jonas Mkude baada ya mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’ kutoa mkwanja mrefu.

0 comments:

Post a Comment

 
Top
CelebritySwaggz.Com