Msanii mwenye mvuto wa kipekee Bongo, Wema Sepetu

ACHANA na umahiri wake awapo bungeni. Weka pembeni sauti yake ya mamlaka na wala usijishughulishe hata kidogo na ujasiri wake wa kumnaga yeyote. Joseph Kasheku ‘King Msukuma’ ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini ametoa ya moyoni na kukiri urembo na ‘figa’ ya msanii Wema Sepetu haupishani na uzuri wa samaki aina ya Nguva, Ijumaa bwana teh…teh… teh…teheeeeee.

Jumatatu ya wiki hii, saa saba na dakika zake mchana, mwandishi wetu akiamini King Msukuma atakuwa nje ya viunga vya bunge akiifaidi posho yake, aliamua kumtafuta kupitia simu yake ya mkononi kwa lengo la kubadilishana naye mawazo juu ya mambo mbalimbali ya kimaendeleo ndipo suala la uhusiano wake na Wema Sepetu likaibukia katikati ya mazungumzo na mbunge huyo kulitolea ufafanuzi.

TULIANZIA HAPA

Siku nne mfululizo za wiki iliyopita, mwandishi wa habari hii alimtafuta mbunge huyo kwa lengo la kufanya naye mahojiano juu ya mambo mbalimbali, ambapo alipokea simu na kusikiliza huku akimuomba mwandishi ampigie baada ya dakika tano kwa kile alichodai… “kuna kitu naweka sawa hapa…”

ATAFUTWA TENA

Baada ya muda huo, mwandishi wetu akiwa na shauku kubwa ya kufanya mahojiano na mbunge huyo machachari ikiwa ni mara yake ya kwanza kuingia bungeni akiwakilisha jimbo jipya, alimpigia simu tena lakini hakupokea, lakini alipotafutwa saa moja usiku siku hiyohiyo, alipokea na kumsikiliza mwandishi wetu kwa kirefu.

AKUBALI KUFANYIWA MAHOJIANO

Muda huo wa saa moja, King Msukuma alikubali ombi la mwandishi ambapo alimuomba ampigie siku iliyofuata (Ijumaa) saa nne asubuhi.

ATAFUTWA, ATOA UDHURU TENA!

Gazeti la Ijumaa huwa halikati tamaa. Siku iliyofuata alitafutwa lakini alimtaka mwandishi wetu amuache kwani alikuwa hospitali akidai kusumbuliwa na tumbo, jambo lililomfanya mwandishi kumpa muda wa kupumzika.

JUMAMOSI NA JUMAPILI ZIII…!

Jitihada za kumtafuta mbunge huyu ziliendelea kwa siku za Jumamosi na Jumapili lakini hakuwa akipokea simu jambo lililoacha maswali mengi kwa mwandishi wetu.

HATIMAYE JUMATATU TIII…!

Sisi nao! Jumatatu ya wiki hii, kama ilivyoelezwa kwenye aya ya pili ndipo mheshimiwa huyo aliweza kuzungumza kwa kirefu na mwandishi wetu ambapo bila kuremba alimtaka aeleze alichofanya jimboni kwake ikiwa ni pamoja na kufungukia madai ya muda mrefu ya kuwahi kuwa ‘close’ sana na msanii Wema Sepetu. Kuhusu mambo ya maendeleo jimboni kwake alimtaka mwandishi wetu avute subira hadi Bunge la Bajeti lipite ndipo atapata muda mzuri wa kukusanya data kamili za utendaji na utimizaji wa ahadi zake jimboni, lakini suala la Wema akalifafanua.

MSIKILIZE MWENYEWE

“Hayo mambo hayawezi kuwa na maana yoyote ya kimaendeleo, muhimu ni kuzingatia utendaji kazi wa mtu na si kutazama mambo ya namna hiyo. Wewe mwenyewe unamuona jinsi huyo mwanamke (Wema) alivyo, mtoto kaumbika kama nguva (aina ya samaki, yaani mtoto ni mashallah na, tena kaumbika namna hiyo, kawaida sana katika maisha,” alisema mheshimiwa huyo.

WEMA ATAFUTWA

Mwandishi wetu pia alifanya jitihada za kumtafuta Wema ili kuzungumzia sifa alizopewa na mheshimiwa huyo lakini kila simu yake ilipopigwa ilikuwa ikiita bila kupokelewa. Hata hivyo, kwa wanawake wengi wamekuwa wakijisikia poa sana wanaposifiwa na wanaume na pia si jambo baya kwa mwanaume kumsifia mwanamke. Kwa maana hiyo alichokifanya Mheshimiwa Msukuma ni kueleza hisia zake, jambo ambalo siyo dhambi hata kidogo.

0 comments:

Post a Comment

 
Top
CelebritySwaggz.Com