KOCHA MSAIDIZI WA SIMBA MGANDA JACKSON MAYANJA.

HUKU wakiwa na imani kuwa ndoto yao ya kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu 2016/17 inaweza kutimia kwa "msaada" wa Fifa, Kocha Msaidizi wa Simba Mganda Jackson Mayanja, amesema timu yake ilikamiwa kuliko timu nyingine kwenye ligi hiyo msimu huu.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mayanja alisema kila mechi kwao ilikuwa ni zaidi ya fainali kwa sababu wapinzani walijipanga "kuzima" ndoto zao za kutwaa ubingwa ambao umekosekana kwa muda mrefu.

Mayanja alisema hali hiyo ilichangia kuwafanya wachezaji wake kutocheza katika viwango vyao vilivyozoeleka katika baadhi ya mechi na kusababisha kupoteza michezo au kutoka sare.

"Tulikuwa na wakati mgumu sana katika kila mechi tuliyocheza, ila tunaamini kila mmoja alifanya kazi yake vizuri, sitaki kuzungumza kiwango cha mchezaji mmoja mmoja, Simba ni timu na hivyo kila kilichopatikana kimetokana na mchango wa kila mmoja wetu," alisema Mayanja.

Nahodha wa timu hiyo, Jonas Mkude, alisema kuwa ligi iliyomalizika ilikuwa ngumu, yenye ushindani na haikuwa kazi rahisi wao kumaliza wakiwa na pointi sawa na mahasimu wao Yanga.

"Kila timu iliyonyesha makali yake, ndiyo maana mpaka siku ya mwisho kulikuwa hakuna bingwa aliyejulikana na timu zilizokuwa zinashuka daraja pia hazikujulikana mapema," Mkude alisema.

Kikosi cha Simba kinatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam leo kuelekea Dodoma kuanza maandalizi ya mchezo wao wa fainali ya Kombe la FA dhidi ya Mbao FC ya Mwanza utakaofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Mshindi katika mechi hiyo atakata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani wakati mabingwa wa Ligi Kuu Bara Yanga wao watashiriki kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

0 comments:

Post a Comment

 
Top
CelebritySwaggz.Com