WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameliagiza Baraza la Madiwani la Manispaa ya Dodoma lifanye marekebisho ya kodi inayotozwa kwenye soko la Majengo ambayo imepandishwa kutoka sh. 20,000 hadi sh. 150,000 kwa mwezi.
 Amesema anatambua maamuzi ya Baraza ni ya kikao halali lakini hakubaliani na ongezeko hilo ambalo ni sawa na asilimia 650 kwani linawaumiza wananchi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Oktoba Mosi, 2016) wakati alipotembelea soko hilo akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma za jamii mjini Dodoma.

Amesema soko hilo linatakiwa lifanyiwe mapitio ili liwekwe kwenye hali nzuri na Manispaa ihakikishe maboresho hayo yanafanyika bila ya kuwaumiza wafanyabiashara.

“Kwa kuwa uamuzi wa kupandisha kodi ulifanyika kisheria na kupitishwa na baraza la Madiwani, sitaki kuvunja sheria. Nawaagiza mkazungumze tena katika baraza na muangalie namna ya kupunguza gharama hizo,” amesema.

“Hali hii haiwezekani kuachwa iendelee, huku ni kuwaumiza wananchi. Mkurugenzi wa Manispaa nenda kaitishe tena kikao, mfanye mazungumzo upya kwenye baraza lenu na mje mnieleze mmekubaliana nini” amesisitiza.

Pia ameitaka Manispaa hiyo ihakikishe makusanyo yote ya fedha katika soko hilo yanakusanywa kwa njia ya kielektroniki ili fedha hizo ziweze kuleta tija na kuwataka Mkuu wa mkoa na wilaya kuwachukulia hatua wotewatakaobainika kuiba fedha hizo.

Amesema Manispaa hiyo inatakiwa kupanua masoko kwa kujenga masoko mapya makubwa katika maeneo ya Nkuhungu, Kisasa, Mlimwa na Barabara ya Iringa ili huduma hizo zisambazwe.

Mapema akisoma risala yake, Mwenyekiti wa soko hilo, Bw. Godson Rugazama alimueleza Waziri Mkuu changamoto zinazolikabili soko hilo kuwa ni pamoja na ongezeko la kodi isiyozingatia uhalisia wa maisha na shughuli za wajasiriamali sokoni hapo. “Kodi imeongezeka kutoka sh. 20,000 hadi 150,000 kwa mwezi,” alisema.

Mwenyekiti huyo alitaja changamoto nyingine ni uchakavu wa mifereji ya maji machafu, kuvuja kwa paa la soko, bidhaa kuuzwa katika maeneo yasiyokuwa rasmi na kusababisha wateja kutoingia sokoni.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu ametembelea hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma na kukagua maeneo mbalimbali zikiwemo wodi za wagonjwa, jengo la wazazi na jengo jipya la wagonjwa wa Bima ya Afya (NHIF).

Akiwa hospitalini hapo, pia alizungumza na watumishi wa sekta ya afya na kuwataka wawahimize wananchi wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao unawawezesha mtu kulipia bima ya matibabu kwa ajili ya mhusika, mwenza wake na watoto/watemezi wanne na serikali inajazia kiasi kile kile alichochangia.

Akizungumzia miundombinu ya afya mkoani humo, Waziri Mkuu alisema mkoa wa Dodoma hauna shida ya matibabu au utoaji wa huduma ya afya kutokana na miundombinu iliyopo hivi sasa.

Aliwataka wafanye kazi kwa uadilifu na uaminifu na kuongeza tija katika utendaji kazi wao huku wakitanguliza utunzaji wa mali ya umma.

“Ninawasihi mjenge tabia ya huruma kwa wagonjwa huku mkitambua unyeti wa kazi mliyonayo. Ninaamini mtatunza vifaa mlivyonavyo na siyo kuvichukua na kuvipeleka kwenye zahanati zenu au maduka yenu binafsi ya dawa,” alionya.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAMOSI, OKTOBA MOSI, 2016

0 comments:

Post a Comment

 
Top
CelebritySwaggz.Com