Kiungo wa zamani wa Yanga, Mrisho Ngassa, ametupa dongo kiaina kwa wachezaji wa Ligi Kuu Bara akiwemo Laudit Mavugo na Method Mwanjale wa Simba, baada ya kutua kwenye klabu yake mpya ya Fanja inayoshiriki Ligi Kuu ya Oman.

Dongo hilo haliishii kwa wachezaji pekee, bali hata kwa timu za hapa nyumbani zenye tabia za kufanya usajili wa wachezaji bila ya kuwapima kama wapo fiti kila idara.

Ngassa amejiunga na timu hiyo hivi karibuni baada ya kuvunja mkataba na Free State ya Afrika Kusini ambapo Fanja imempa mkataba wa miaka miwili sambamba na straika, Danny Lyanga aliyekuwa Simba.

Kiungo huyo mshambuliaji siku chache baada ya kujiunga na timu hiyo, ametupia picha kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram ikionyesha vipimo alivyofanyiwa huku akiandika: “Na Bongo wapimwe kabla ya kusajiliwa.”

Kwa mujibu wa picha hiyo, inaonyesha vipimo vyake alifanyiwa Septemba 21, mwaka huu kwenye Hospitali ya Badr Al Samaa chini ya daktari, Meena Paul, yupo fiti na hana tatizo lolote.


Ikumbukwe kuwa, utaratibu huo wa kuwapima wachezaji kabla ya kusajiliwa umekuwa mgumu kwa hapa nyumbani kwani mara kadhaa wachezaji wanasajiliwa kimagumashi na mwisho wa siku wanakuja kugundulika wana matatizo ya afya.

0 comments:

Post a Comment

 
Top
CelebritySwaggz.Com