Mwigizaji Kajala Masanja. Niko nje ya nyumba nzuri, iliyobadikwa kibao kinachosomeka; ‘Inalindwa na Nyangumi Security’ nikashtuka kidogo lakini nikagonga geti na kufunguliwa na macho yangu yakakutana na mdada mrembo, amevaa shati la kukata mikono na chini amejifunga khanga huku mkononi ameshika glasi ya juisi.
Akaachia tabasamu kuikaribisha Mpaka Home, tukaingia ndani kwa mwigizaji Kajala Masanja anayeishi maeneo ya Sinza Afrikasana, jijini Dar.
Kama ilivyo desturi ya Mpaka Home kuwatembelea mastaa mbalimbali na kujua maisha yao binafsi, Kajala naye aliulizwa mambo anayoyafanya akiwa nyumbani na majibu yake yalikuwa kama ifuatavyo:

MAISHA YAKE YA KAWAIDA YAPOJE?
“Maisha yangu nje ya sanaa ni ya kawaida sana ni kama wanavyoishi binadamu wengine, tena maisha ya  kawaida mno kikubwa ninapenda kuishi sehemu ambayo haina kelele wala fujo kwa sababu kuna kipindi nasumbuliwa na kichwa sana hivyo najisikia amani nikikaa sehemu tulivu.

NI MTAALAMU WA JIKO?
“Mimi na jiko ni kama mtu na rafiki yake kwa sababu napenda sana kula chakula ambacho nakiwazia kichwani kwangu hivyo ili nile chakula ambacho ninakitaka, lazima niingie jikoni nikipike mwenyewe  ila nikiwa nimechoka dada wa nyumbani anaweza kunipikia kwa kuwa nimemuelekeza hivyo anajua napenda nini.

NI NINI SEHEMU KUBWA YA MAISHA YAKE?
“Kwa sasa nina vitu vikubwa viwili kwenye maisha yangu; kwanza kabisa napenda kusali na hata ukiingia chumbani kwangu ninapolala huwezi kukosa Biblia na vitabu vya nyimbo za dini lakini kingine ni mazoezi ambayo kiukweli yamenifanya niwe vizuri kwa sababu nilikuwa nasumbuliwa na tatizo la moyo hivyo mazoezi yamenisaidia sana.

ANAZUNGUMZIAJE CHUMBA CHAKE?
“Chumba changu cha kulala ndiyo sehemu moja kubwa sana naiheshimu hapa nyumbani kwangu, nakipa chumba changu hadhi kubwa sana, siyo rahisi kuona mtu anaingia hovyohovyo labda saa ya kufanyiwa usafi na mara nyingi sipendagi kulala na mtu chumbani kwangu ndiyo nimejizoesha hivyo hata akirudi mwanangu (Paula, yupo bording) ana chumba chake.
ANAMZUNGUMZIAJE MTOTO WAKE PAULA?
“Nampenda sana lakini watu wengi hunilaumu kwa nini namvalisha nguo fupi na vitu vingine lakini kitu ambacho hawakijui mimi ni mama wa tofauti sana, kuna nafasi yangu ya mama ambayo hata yeye anatambua hawezi kufanya mzaha kwenye hilo.

NINI ANACHOKITAMANI KWA SASA?
“Natamani nikitoka hapa ninapoishi nisipange nyumba tena, natamani niende kuishi kwenye nyumba yangu.

VIPI KUHUSU UPWEKE?
“Upweke ni lazima kwa mwanamke ambaye tayari ameshaolewa, natamani kuwa na mume wangu maana mnapoishi wawili na kuishi mmoja ni vitu viwili tofauti kabisa lakini najitahidi kujipooza kwa kuangalia tamthiliya na vitu mbalimbali vya kunipoteza mawazo.
Kuipata Mpaka Home yote ya Kajala ingia www.globaltvtz.com ili upate uhondo zaidi

0 comments:

Post a Comment

 
Top
CelebritySwaggz.Com