Taasisi ya T.Marc Tanzania, ambayo iliendesha mashindano ya Dume Challenge imeeleza kushtushwa na kusikitishwa na taarifa za kukamatwa kwa Salum Njwete, maarufu kwa jina la Scorpion.

Taasisi hiyo pia imethibitisha kuwa Njwete alishiriki na kushinda mashindano ya Dume Challenge Season 1 mwaka 2012 na kuwa balozi wa kondomu za taasisi hiyo chapa ya Dume kuanzia mwaka 2012 hadi 2014.

Njwete alikamatwa na kushtakiwa kwa uporaji wa kutumia silaha na kumjeruhi baada ya wananchi kulalamika kwenye vyombo vya habari kuwa kuna mtu anayeitwa Scorpion aliyekuwa akipora na kujeruhi wananchi, akiwemo kinyozi Said Ally wa Mabibo Hosteli aliyeporwa fedha na kutobolewa macho.

“Hata hivyo, tangu mwaka 2014, Bwana Njwete hajakuwa na uhusiano na chapa hiyo,” inasema taarifa ya T-Marc iliyosainiwa na mkurugenzi mkuu, Diana Monika Kisaka.

“T-Marc pia inapenda kuthibitisha kuwa Bwana Njwete alikuwa balozi wa programu ya kuwezesha wasichana ya “Hakuna wasichoweza” mwaka 2014 ambayo imeisha muda.

“T-Marc haina tena uhusiano wa aina yoyote, rasmi au kwa njia yoyote ile na Njwete. T-Marc inaamini kuwa haki itatendeka katika shauri ambalo Njwete anatuhumiwa.”

Taasisi hiyo imesema inaendelea kujikita katika kutoa huduma kwa maisha ya Watanzania kwa kutoa bidhaa na programu bora.

0 comments:

Post a Comment

 
Top
CelebritySwaggz.Com