Hofu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kumfutia dhamana Tundu Lissu ambaye ni mtuhumiwa wa kesi ya uchochezi, imetoweka baada ya mahakama hiyo kukubaliana na utetezi wa  wadhamini wake kuwa, Lissu yupo Ujerumani kwa matibabu.

Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Mbunge wa jimbo la Singida Mashariki, alishindwa kuhudhuria mahakamani siku ya juzi na hivyo wadhamini wake kutakiwa kufika mahakamani jana kujieleza, kwanini mtuhumiwa huyo asifutiwe dhamana.

Kesi ya uchochezi inayomkabili Lissu ni kesi Na. 208 katika gazeti la MAWIO akiwa ni mtuhumiwa namba nne sambamba na Jabir Idrissa, Simon Mkina, na Ismail Merhaboob.

Jabir ni mwandishi mwandamizi wa MAWIO, Mkina ni mhariri wa gazeti hilo na Merhaboob ni meneja wa kampuni ya uchapishaji magazeti inayojulikana kwa jina la Flint.
Jana, wadhamini wa Lissu Ibrahim Ahmed na Robert Katula walisimama mbele ya Hakimu Thomas Simba anayesimamia kesi hiyo, na kusema kuwa Lissu hakutokea  mahakamani kwa sababu amesafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Hata hivyo, upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Mutalemwa Kisheruji uliiomba mahakama kuzuia hati ya kusafiria ya mshitakiwa Lissu pamoja na kumuwekea sharti la kuiomba mahakama kibali cha kusafiria endapo atarudia tena kosa hilo kutokana kwamba hakufuata sheria kwa sababu alitakiwa kutoa taarifa mapema kabla ya siku ya shtaka kusikilizwa.

Lakini Hoja hiyo ilipingwa na Wakili wa upande wa utetezi Peter Kibatala na kuiomba mahakama kutenga siku nyingine ambapo alimuahidi hakimu kuwa kosa hilo halitajirudia tena na siku husika ya kusikilizwa shitaka mshatikiwa atakuja mahakamani.

Baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili, Hakimu Simba alitoa onyo kali kwa mshitakiwa na kuwaambia wadhamini wa Lissu kuwa, endapo siku nyingi mshitakiwa huyo hatakuja mahakamani, wadhamini watalipa dhamana.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba, 4, 2016 baada ya mawakili wa pande zote mbili kuiridhia tarehe hiyo iwe siku ya kusikilizwa shtaka hilo.

0 comments:

Post a Comment

 
Top
CelebritySwaggz.Com