Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu. Huu ni msemo ambao naanza nao siku ya leo kutokana mwenendo mbaya wa maisha ya msanii mahiri Hip Hop, David Genzi aka ‘Young Dee’.

Wiki hii kumekuwa na picha pamoja na video ambazo zinasambaa katika mitandao ya kijamii zikimuonyesha Young Dee ‘Rapper Paka’ akivutana na watu wanaodaiwa kuwa ni polisi na baadaye kutiwa mbaroni kwa madai ya kumshambulia jirani yake wa kike maeneo ya Sinza anakoishi na kisha kumvunjia simu yake ya mkononi.

Tukio hili limeibua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii huku mashabiki wa muziki wake wakishangazwa na style ya maisha ya Young Dee ikiwa miezi michache toka agombane na kuachana na meneja wake, Max Rioba.

Tusiingie ndani sana kuzungumzia ugomvi wake na meneja wake huyo ambaye alishirikiana naye kutengeneza hits kadhaa ambazo bado zinampatia jeuri ya kuishi mjini. Lakini kauli ambayo aliitoa meneja wake wakati wanaachana “Kama usiposhtuka sasa hivi na kugundua kuwa huna hata chumba cha kupanga au hata begi la nguo halafu unajiita msanii wa muziki utastuka when it’s very late. Washkaji zako wote ni wahuni, bangi, cocaine, pombe na mademu wasiojua hata kuandika aeiou. Hayo sio maisha!. Hii ni kauli ambayo inaendelea kumtafuna Young Dee.

Kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na Matumizi ya Madawa ya kulevya japokuwa amekuwa akitumia nguvu kubwa kulikanusha suala hilo mpaka kuamua kuandika wimbo ‘Fununu’ ambao ndani yake aliendelea kuuthibishia umma kwamba hatumii madawa ya kulevya. Lakini matendo na mwonekano wake bado vinawapa watu sababu za kumshuku kwamba anatumia madawa ya kulevya.

Huu ni wakati wa Young Dee kubadilika na kufungua ukurasa mpya wa maisha yake, ajifunze kutokana kaka yake kama TID ambaye mwaka 2008, alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kutiwa hatiani kwa kujeruhi. Nadhani hili lingekuwa funzo zuri kwake kwa kuamini hakuna aliyejuu ya sheria.
Young Dee ana nafasi ya kufanya vizuri zaidi kimuziki na kufika mbali zaidi, lakini kama akiweza kutoka katika kifungo cha kauli ya aliyekuwa meneja wake, Max Rioba.

0 comments:

Post a Comment

 
Top
CelebritySwaggz.Com