Wakati Polisi ikimshikilia kwa saa mbili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe mkoani Mwanza, jeshi hilo limefuta kongamano la kujadili Bajeti ya Serikali lililoandaliwa na ACT Wazalendo jijini Dar es Salaam huku kiongozi wake, Zitto Kabwe akisakwa.

Jeshi hilo lilizuia mkutano wa hadhara wa Chadema uliokuwa ufanyike wiki iliyopita mjini Kahama ambako lilitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanachama na wafuasi wa chama hicho, katika kile kilichoelezwa kulikuwa na dalili za uvunjifu wa amani.

Jeshi hilo pia lilizuia msafara wa viongozi wa chama hicho kuingia katika ofisi zake za Shinyanga walipokuwa wakielekea Mwanza.

Taarifa iliyotolewa jana na msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene ilieleza kuwa mbali na Mbowe, jeshi hilo pia lilikuwa linawashikilia Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi na Katibu Mkuu wa Bavicha, Julius Mwita.

Wengine ni Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka na viongozi wengine na wanachama wa chama hicho waliokuwa wanashikiliwa katika kituo cha Polisi Nyakato, jijini Mwanza.

Makene alisema tangu asubuhi ya jana, Mbowe na viongozi wenzake walikuwa wakizunguka katika maeneo kadhaa ya jijini Mwanza kuwasalimia wananchi katika ‘vijiwe’ mbalimbali kabla hawajakamatwa.

Alisema, “Hadi sasa (saa 11 jioni) hakuna maelezo ya kushikiliwa kwao.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alithibitisha kukamatwa kwa viongozi hao na kubainisha kuwa waliachiwa bila kufunguliwa kesi yoyote.

“Walikutwa Igoma Sokoni wakizungumza na wananchi. Mikutano ya namna hii imezuiwa. Wamefungua kesi mahakamani, hivyo hakuna haja ya kufanya tofauti mpaka itakapohukumiwa,” alisema Msangi.

Alifafanua kuwa jeshi hilo halina uhasama wowote na Chadema au chama kingine chochote na "hatuwezi kukiingilia kinapofanya mikutano yake ya ndani au hotelini. Kilichozuiwa ni mikutano ya hadhara.”

Wakati Msangi akisema hayo, kongamano la ACT Wazalendo ambalo lilitakiwa lifanyike jana kuanzia saa 7:00 mchana kwenye Ukumbi wa Jengo la LAPF; Millennium Towers, Kijitonyama lilizuiwa na polisi.

Tangu mapema asubuhi, askari polisi walitanda katika eneo la ukumbi huo kuzuia kongomano hilo.

Ukumbini hapo, waandaaji walisema hakuna anayeruhusiwa kuingia kwani wamepewa maelezo ya kuufunga baada ya tukio lililoandaliwa kuahirishwa.

Zaidi ya viti 210 vilikuwa vimepangwa kwa ajili ya kongamano hilo na mmoja wa viongozi wa ukumbi huo alionekana akiondoa mabango yaliyokuwa yanautambulisha mkutano huo wa ACT.

Viongozi watatu wa ukumbi huo walikataa kueleza kinagaubaga juu ya sakata hilo, lakini taarifa za jumla zilisema mkutano umezuiwa.

Mmoja wa watumishi wa ukumbi huo, alisema: “Tuliandaa kila kitu, ila shughuli imeahirishwa. Ukumbi unatakiwa kufungwa. Hautatumika kwa leo.”

Ilipofika saa 5:00 asubuhi, Msemaji wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis alisema chama kinafanya mkutano wa dharura kwenye ofisi zake za makao makuu na baadaye kingezungumza na waandishi wa habari.

Saa 8:00 mchana, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Anna Mghwira akiwa na viongozi wenzake, isipokuwa Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe alikuwa mbele ya kamera za wanahabari akifafanua kilichotokea kwa wanachama, wafuasi wa chama hicho na Watanzania kwa ujumla.

Alisema ilipotimu saa 4:00 asubuhi walipewa taarifa na mwenye ukumbi kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni limemjulisha kuwa chama hicho hakina kibali cha kuendesha kongamano hilo na kwamba kisiruhusiwe kufanya hivyo.

“Huku ni kufifisha demokrasia. Wapigania haki za kiraia wasimame imara na vyama vya upinzani katika kuilinda,” alisema Mghwira.

Wakati kongamano hilo likizuiwa, kuna taarifa za kukanganya juu ya alipo Zitto baada ya kudaiwa alikuwa anasakwa na polisi tangu juzi.

Taarifa hizo zinakuja siku chache baada ya kiongozi huyo kuitwa Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam na kuhojiwa juu ya kauli alizozitoa kwenye mkutano wa hadhara zinazokosoa utendaji wa Serikali na kupinga matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar.

Baadaye jioni, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Msafiri Mtemelwa alitoa taarifa kuwa Zitto ametoweka na hajulikani alipo. Hiyo ilikuwa ni baada ya askari kanzu kumtafuta kwa muda kwa saa kadhaa.

“Zitto amekuwa akitafutwa kwa muda mrefu. Askari wanalinda nyumbani kwake tangu jana (juzi) usiku. Hivi sasa ametoweka, hatujui alipo. Lolote litakalompata, Jeshi la Polisi litajibu,” alisema Mtemelwa.

Awali, Mghwira alipoulizwa imekuwaje kuhusu Zitto alijibu kuwa mkutano ulikuwa wa dharura ndiyo maana viongozi wote hawakuwapo.

0 comments:

Post a Comment

 
Top
CelebritySwaggz.Com