Jina la Black Coffee, Sio jina linalotambulika sana miongoni mwa watanzania. Mimi binafsi nilianza kufuatilia kazi zake baada ya kutajwa kuwa miongoni mwa wanamuziki wanaowania tuzo za BET za mwaka huu katika kipengele cha Best International Act-Africa akiwemo Diamond Platinumz. Nikiri kwamba sikumfahamu mpaka mapema mwaka huu.
Haishangazi kuona kwamba baada ya kushinda tuzo ya BET katika kipengele cha Best International Act-Africa hapo jana, watanzania wengi hatukuamini. Wengine walighafilika kabisa na kufanya kitendo ambacho naweza kukiita sio cha kiungwana. Baadhi waliingia kwenye kurasa za Instagram za Black Coffee na BET Africa na kubwaga mioyo yao.
Walioingia kwenye ukurasa wa BET Africa na kuelezea hisia zao,siwezi kuwalaumu sana. Unaposhindana unategemea kushinda.Ukishindwa habari ya asiyekubali kushindwa sio mshindani,huweza kuyeyuka. Cha ajabu ni tulipoamua kumwagia upupu wa kejeli na matusi Black Coffee kwenye kurasa zake binafsi. Yeye katangazwa mshindi. Akatae? Kosa lake lipo wapi? Kahonga ili ashinde?
Kitendo kile sio cha kiungwana hata kidogo. Tulitakiwa kuelezea hisia zetu kwa staha,ustaarabu na uungwana. Vinginevyo tunahatarisha kuwaharibia wasanii wetu hata teuzi za mbeleni. Na wala sio jambo baya kumpongeza mshindi. Ndio ushindani wa kweli. Unapokwenda kushindana, kuna kushinda na kushindwa. Tumeshawahi kushinda. Hatukumiminiwa matusi. Kwanini kwetu iwe tofauti?
Lakini Black Coffee ni nani? Iweje ashinde tuzo za BET ilhali wewe humfahamu au hujawahi kusikia kazi zake kabla ya jana? Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya mtandaoni ikiweko Wikipedia na vyombo vya habari vya Afrika Kusini na kwingineko duniani, jina lake kamili ni Nkosinathi Innocent Maphumulo na alizaliwa tarehe 11 March 1976 huko eThekwini, Durban.
Black Coffee BET Awards Best International Act 2016-Winner
Alianza kujishughulisha rasmi na muziki mwaka 1995 kama DJ na Producer. Mpaka sasa ana albums 5. Kama unapenda kazi za David Guetta wa Ufaransa unaweza kufananisha anachokifanya Black Coffee na DJ huyo na wengine duniani kama DJ Khaled nk.
Inaaminika kwamba kwa upande wa Africa, Black Coffee ni miongoni mwa DJs na Producers mabingwa. Huko Afrika Kusini ameshashinda tuzo kadhaa ikiwemo ya mwaka 2015 ya Breakthrough DJ Of The Year katika tuzo za DJs (DJ Awards) zilizofanyikia Ibiza, Spain. Tuzo hiyo ilifuatia kutoa album yake ya 5 ya Pieces Of Me. Black Coffee pia anamiliki record label Soulistic Music. Ameshashinda tuzo nyingine kadhaa zikiwemo za South Africa Music Awards(SAMA) na Chanel O.
Kwa hiyo ukiangalia kutokea alipoanza mwaka 1995 mpaka hapa alipofikia hivi sasa ni kwamba amepitia mengi ikiwemo kushindanishwa, kushinda na kushindwa. Historia yake inasema kuteuliwa kwake kushiriki katika Red Bull Music Academy mwaka 2004 huko Cape Town ndiko kulimuweka kwenye ramani ya dunia. Red Bull Music Academyni jukwaa la kimataifa la kuvumbua vipaji. Naamini pale ndipo alipojiweka “kimataifa”. Ni njia muhimu.
Kama wanamuziki wengine wanavyofanya, ili ujulikane kimataifa unaweza pia kushirikiana na wasanii wengine wakubwa duniani. Kwa bahati nzuri au mbaya, yeye hakuhitaji kwenda mbali sana nje ya Afrika Kusini ambapo kuna majina kama Hugh Masekela, Busi Mhlongo,DJ Shimza, Yvonne ChakaChaka nk.
Katika kushirikiana na majina hayo makubwa, mwaka 2005 Black Coffee aliufanyia DJ sampling wimbo maarufu wa Hugh Masekela uitwao Stimela (1972). Hugh Masekelani legend wa Afrika. Alimshirikisha katika album yake ya kwanza aliyoipa jina lake Black Coffee. Unaweza kuona jinsi gani wimbo huo ulimsaidia Black Coffee.
Kabla ya hapo alienda shule kusomea muziki wa Jazz katika chuo cha muziki chaTechnikon Natal. Na kabla ya hapo alikuwa miongoni mwa waimbaji wasaidizi wa Madala Kunene pamoja na wanafunzi wenzake wanafunzi wenzake, Mngobi Mdabe(Shota) na Thandukwazi Sikhosana(Demor).Madala Kunene ni miongoni mwa wanamuziki wa Afrika wanaosifika kwa kupiga muziki wa Afrika asilia. Vibao vya Kunene kama vile UbomboMlisaAbangoma nk vinaweza kukupa picha ya alipotoka Black Coffee.
Baadae akishirikiana na Mngobi Mdabe(Shota) na Thandukwazi Sikhosana(Demor) waliunda kundi la muziki wa Afro-Pop walilolipa jina SHANA ikiwa ni kifupi cha Simply Hot and Naturally African. Baadae aliamua kwenda kivyake.
Kingine ambacho naamini kimemfikisha Black Coffee hapa alipofika ni “branding”.Ukimfuatilia kwenye tovuti yake rasmi, kwa mfano, utaona kwamba amejiweka kibiashara haswa..Ni kama vile anajiandaa kufika mahali fulani. Huwezi kuwa msanii hivi leo halafu ukawa huna tovuti inayoeleweka.Inaonekana wazi kabisa kwamba nyuma yake wapo watu makini sana wanaosimamia kazi zake au kushirikiana naye.
Kingine ambacho bila shaka BET Awards Academy wamekiona ni jinsi ambavyo Black Coffee katika nyimbo zake anajaribu sana kuhifadhi ile ladha ya muziki wa kiafrika au tuseme wa Afrika Kusini. Originality ni miongoni mwa vitu vinavyozingatiwa na kuheshimiwa sana katika utoaji wa tuzo.
Red Bull Taster ZA 09
Kwa hiyo unaweza kuona kwamba kushinda kwake tuzo ya BET sio ajali kubwa kuliko zingine zozote kuwahi kutokea. Hatujashindwa na bwege. Lipo la kujifunza. Na kwa namna moja au nyingine (ingawa hata mimi nilitamani Diamond Platinumz ashinde) hakushinda kwa ngekewa tu.
Kinachotia moyo ni kwamba mwanetu Diamond Platinumz haonyeshi kubeza hata kidogo kazi za Black Coffee. Kupitia ukurasa wake wa Instagram amempongeza na kumtakia kila la kheri. Huo ndio uungwana na moyo wa ushindani. Anajua kuna mwakani na kuna tuzo zingine. Ushindi upo tu. Isitoshe kama video zetu karibu zote tunafanyia South Afrika siku hizi, uadui hauwezi kutusaidia.
Black Coffee na mkewe Mbali Mlotshwa
Mwaka 2011 Black Coffee alimuoa mwigizaji na mtangazaji wa televisheni, Mbali Mlotshwa. Wana watoto wanne Esona, Lilitha, Anesu na Asante. Wawili kati ya hao ni kutoka kwenye mahusiano yake kabla ya kumuoa Mbali.
Ratiba yake inaonyesha kwamba kuanzia mwezi ujao wa Julai mpaka October ana tour katika nchi za Marekani, Spain, Switzerland, Germany, Greece,Belgium na Afrika Kusini. Mwaka huu tayari ameshiriki katika matamasha makubwa ya muziki dunianiCoachella Valley Music and Arts Festival na Ultra Music Festival.
Hatujashindwa na bwege. Tunalo la kujifunza.
cc: Jeff Msangi

0 comments:

Post a Comment

 
Top
CelebritySwaggz.Com